Taswira ya Vijana kama Mkakati wa Kuibua Falsafa ya Mwandishi: Tathmini ya Riwaya za G. K. Mkangi Walenisi (1995) na Mafuta (1984).
Publication Date
2024Author
Type
ArticleMetadata
Show full item record
Abstract/ Overview
Utafiti unaonyesha kwamba, vijana kote duniani sasa wana utamaduni wao ambao watafiti wanaueleza kama ‘ulimwengu huru’ wa vijana ulio na mitindo na njia za maisha ambazo vijana hufuata ili kujitofautisha na utamaduni wa wazazi wao. Utamaduni wa vijana kwa kiasi kikubwa ni zao la maendeleo katika jamii za ulimwengu. Kadri jamii inavyosonga mbele kimaendeleo, ndivyo ambavyo utamaduni wa vijana unakuzwa, unaimarishwa na kusambazwa miongoni mwa vijana kote duniani. Vijana wamebuni utamaduni wao kama njia moja ya kuasi dhidi ya utamaduni uliotawaliwa na wazee. Wanataka kujihusisha na tabia kama matumizi ya dawa za kulevya, ushoga, uasi wa maadili ya kijamii, mitindo mipya ya mavazi, muziki miongoni mwa tabia nyingine ambazo wanajua huwatenga wazee. Hii ni tabia ibuka ya vijana kupania kuonyesha nguvu na uwezo wao katika jamii. Ujumbe wanaopitisha ni kuwa, hawako tayari kushiriki utamaduni unaowadhibiti na kuwanyima nafasi yao katika jamii. Data ya utafiti huu ilipatikana maktabani ambapo vitabu teule, majarida, tasnifu na maandishi muhimu yanayohusiana na mada ya utafiti yalisomwa na data ya msingi na upili kunukuliwa. Makala hii iliongozwa na malengo mawili. Moja kudadavua taswira mbalimbali za vijana katika riwaya teule na ya pili kubainisha falsafa ya mwandishi Mkangi kupitia taswira ya vijana katika riwaya hizi mbili Makala hii inapanga kuangazia taswira ya vijana wa kisasa katika riwaya ya Mafuta na Walenisi ili vijana waweze kuzinduka na kubadilisha hali yao ya kimaisha. Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kwamba, Matumizi mbalimbali ya taswira kuhusu vijana yanamwezesha Mkangi kuibua falsafa yake kuhusiana na suala la vijana katika jamii zetu na wakati huohuo kutaka kuzindua umma mkubwa wa vijana unaolala ili waweze kuamka na kubadilisha hali yao ya maisha katika dunia hii inayobadilika kila uchao.